Mika 6 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Shtaka la Mwenyezi Mungu dhidi ya Israeli

1Sikiliza asemalo Mwenyezi Mungu:

“Simama, jitetee mbele ya milima;

vilima na visikie lile unalotaka kusema.

2“Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya Mwenyezi Mungu,

sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ana shauri dhidi ya watu wake;

anatoa mashtaka dhidi ya Israeli.

3“Watu wangu, nimewatendea nini?

Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu.

4Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa

kutoka nchi ya utumwa.

Nilimtuma Musa awaongoze,

pia Haruni na Miriamu.

5Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu

alivyofanya shauri

na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu.

Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu hadi Gilgali,

ili mfahamu matendo ya haki ya Mwenyezi Mungu.”

6Nimjie Mwenyezi Mungu na kitu gani na kusujudu

mbele za Mungu aliyetukuka?

Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,

nije na ndama za mwaka mmoja?

7Je, Mwenyezi Mungu atafurahishwa na kondoo dume elfu,

au mito elfu kumi ya mafuta?

Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza

kwa ajili ya kosa langu,

mtoto wangu mwenyewe

kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?

8Amekuonesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

Mwenyezi Mungu anataka nini kwako?

Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

Hatia na adhabu ya Israeli

9Sikiliza! Mwenyezi Mungu anauita mji:

kulicha jina lako ni hekima:

“Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru.

10Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu,

hazina yako uliyopata kwa udanganyifu

na vipimo vilivyopunguka,

ambavyo vimelaaniwa?

11Je, naweza kuhukumu kuwa

mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia,

aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?

12Matajiri wake ni wajeuri;

watu wake ni waongo

na ndimi zao zinazungumza

kwa udanganyifu.

13Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu,

kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.

14Mtakula lakini hamtashiba;

tumbo zenu bado zitakuwa tupu.

Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote,

kwa sababu mtakachoweka akiba

nitatoa kwa upanga.

15Mtapanda lakini hamtavuna;

mtakamua zeituni lakini

hamtatumia mafuta yake.

Mtakamua zabibu

lakini hamtakunywa hiyo divai.

16Mmezishika sheria za Omri

na matendo yote ya nyumba ya Ahabu,

tena umefuata desturi zao.

Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi

na watu wako kuwa dhihaka;

mtachukua dharau za mataifa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help