Isaya 11 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Tawi kutoka kwa Yese

1Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,

kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.

2Roho wa Mwenyezi Mungu atakaa juu yake,

Roho wa hekima na wa ufahamu,

Roho wa shauri na wa uweza,

Roho wa maarifa na wa kumcha Mwenyezi Mungu

3naye atafurahia kumcha Mwenyezi Mungu.

Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,

wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

4bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,

kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.

Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,

kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

5Haki itakuwa mkanda wake

na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

6Mbwa-mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

naye chui atalala pamoja na mbuzi,

ndama, mwana simba na ng’ombe wa mwaka mmoja

watakaa pamoja,

naye mtoto mdogo atawaongoza.

7Ng’ombe na dubu watalisha pamoja,

watoto wao watalala pamoja,

na simba atakula majani makavu kama maksai.

8Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,

naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

kwenye kiota cha fira.

9Hawatadhuru wala kuharibu

juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Mwenyezi Mungu

kama maji yajazavyo bahari.

10Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.

11Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi, na kutoka visiwa vya baharini.

12Atainua bendera kwa mataifa

na kuwakusanya Waisraeli walio uhamishoni;

atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika

kutoka pembe nne za dunia.

13Wivu wa Efraimu utatoweka,

na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;

Efraimu hatamwonea Yuda wivu,

wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.

14Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti

hadi upande wa magharibi,

kwa pamoja watawateka watu nyara

hadi upande wa mashariki.

Watawapiga Edomu na Moabu,

na Waamoni watatawaliwa nao.

15Mwenyezi Mungu atakausha

ghuba ya bahari ya Misri;

kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake

juu ya Mto Frati.

Ataugawanya katika vijito saba

ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.

16Kutakuwa na njia kuu kwa mabaki ya watu wake

wale waliosalia kutoka Ashuru,

kama ilivyokuwa kwa Israeli

walipopanda kutoka Misri.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help