Yona 2 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Maombi ya Yona na kuokolewa

1Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Yona alimwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wake.

2Akasema:

“Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu,

naye akanijibu.

Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada,

nawe ukasikiliza kilio changu.

3Ulinitupa kwenye kilindi,

ndani kabisa ya moyo wa bahari,

mikondo ya maji ilinizunguka;

mawimbi yako yote na viwimbi

vilipita juu yangu.

4Nikasema, ‘Nimefukuziwa

mbali na uso wako,

hata hivyo nitatazama tena

kuelekea Hekalu lako takatifu.’

5Maji yaliyonimeza yalinitisha,

kilindi kilinizunguka;

mwani ulijisokota kichwani pangu.

6Nilizama chini sana hata pande za mwisho za milima,

makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele.

Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni,

Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.

7“Uhai wangu ulipokuwa unatoka,

nilikukumbuka wewe, Mwenyezi Mungu,

nayo maombi yangu yalikufikia wewe,

katika Hekalu lako takatifu.

8“Wale watu wanaoshikilia sanamu batili

hupoteza neema yao.

9Lakini mimi nitakutolea dhabihu,

kwa sauti za shukrani na shangwe.

Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza.

Wokovu watoka kwa Mwenyezi Mungu.”

10Basi Mwenyezi Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help