Zaburi 31 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 31Maombi na sifa kwa kuokolewa kutoka kwa aduiKwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe,

usiache nikaaibika kamwe,

kwa haki yako uniokoe.

2Nitegee sikio lako,

uje uniokoe haraka;

uwe kwangu mwamba wa kimbilio,

ngome imara ya kuniokoa.

3Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu,

uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.

4Uniepushe na mtego niliotegewa,

maana wewe ndiwe kimbilio langu.

5Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,

unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli.

6Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili;

bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu.

7Nitafurahia na kushangilia upendo wako,

kwa kuwa uliona mateso yangu

na ulijua maumivu ya nafsi yangu.

8Hukunikabidhi kwa adui yangu

bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.

9Ee Mwenyezi Mungu unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;

macho yangu yanafifia kwa huzuni,

nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.

10Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,

naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;

nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,

na mifupa yangu inachakaa.

11Kwa sababu ya adui zangu wote,

nimedharauliwa kabisa na majirani zangu,

hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho,

wale wanaoniona barabarani wananikimbia.

12Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,

nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.

13Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi;

vitisho viko pande zote;

kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu,

na kula njama kuniua.

14Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu;

nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”

15Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,

uniokoe mikononi mwa adui zangu

na wale wanifuatiao.

16Mwangazie mtumishi wako uso wako,

uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.

17Usiniache niaibike, Ee Mwenyezi Mungu,

kwa maana nimekulilia wewe,

bali waovu waaibishwe

na kunyamazishwa Kuzimu.

18Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,

kwa maana kwa kiburi na dharau

wao husema kwa majivuno

dhidi ya wenye haki.

19Tazama jinsi wema wako ulivyo mkuu,

uliowawekea akiba wanaokucha,

unaowapa wale wanaokukimbilia

machoni pa watu wote.

20Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako

kutokana na hila za wanadamu;

katika makao yako huwaweka salama

kutokana na ndimi za mashtaka.

21Atukuzwe Mwenyezi Mungu,

kwa kuwa amenionesha upendo wake wa ajabu

nilipokuwa katika mji uliozingirwa.

22Katika hofu yangu nilisema,

“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”

Hata hivyo ulisikia kilio changu

ukanihurumia nilipokuita unisaidie.

23Mpendeni Mwenyezi Mungu ninyi watakatifu wake wote!

Mwenyezi Mungu huwahifadhi waaminifu,

lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.

24Kuweni hodari na mjipe moyo,

ninyi nyote mnaomtumaini Mwenyezi Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help