Ezekieli 27 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Maombolezo kwa ajili ya Tiro

1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:

2“Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro.

3Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:

“ ‘Ee Tiro, wewe umesema,

“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”

4Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,

wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.

5Walizifanya mbao zako zote

kwa misunobari kutoka Seniri;

walichukua mwerezi kutoka Lebanoni

kukutengenezea mlingoti.

6Walichukua mialoni kutoka Bashani

wakakutengenezea makasia yako;

kwa miti ya msanduku

kutoka pwani ya Kitimu

wakatengeneza sitaha yako

na kuipamba kwa pembe za ndovu.

7Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,

nacho kilikuwa bendera yako;

chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau

kutoka visiwa vya Al-Yasa.

8Wakaaji wa Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;

watu wako wenye ustadi, ee Tiro,

ndio walikuwa mabaharia wako.

9Wazee wa Gebali pamoja na mafundi stadi

walikuwa mafundi wako kwenye meli.

Meli zote za baharini na mabaharia wao

walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.

10“ ‘Wanaume wa Uajemi, Ludi na Putu

walikuwa askari katika jeshi lako.

Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,

wakileta fahari yako.

11Watu wa Arvadi na wa Heleki

walikuwa juu ya kuta zako pande zote;

watu wa Gamadi

walikuwa kwenye minara yako.

Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;

wakaukamilisha uzuri wako.

12“ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali yako.

13“ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki walifanya biashara nawe; walibadilisha binadamu na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.

14“ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali yako.

15“ ‘Watu wa Dedani walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.

16“ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu.

17“ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walibadilishana ngano iliyotoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri kwa bidhaa zako.

18“ ‘Dameski walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako na ukuu wa utajiri wa mali zako, wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.

19“ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali walikuletea mali ya biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.

20“ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.

21“ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako; walifanya biashara nawe ya kubadilishana wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.

22“ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezo, vito vya thamani na dhahabu.

23“ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe.

24Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.

25“ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo

zinazokusafirishia bidhaa zako.

Umejazwa shehena kubwa

katika moyo wa bahari.

26Wapiga makasia wako wanakupeleka

mpaka kwenye maji makuu.

Lakini upepo wa mashariki utakuvunja vipande vipande

moyoni mwa bahari.

27Utajiri wako, bidhaa zako na mali yako,

mabaharia wako, manahodha wako,

mafundi wako wa meli,

wafanyabiashara wako na askari wako wote,

na kila mmoja aliye kwenye meli

atazama kwenye moyo wa bahari

siku ile meli yako itakapovunjika.

28Nchi za pwani zitatetemeka

wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.

29Wote wapigao makasia

wataacha meli zao,

mabaharia wote na wanamaji wote

watasimama pwani.

30Watapaza sauti zao

na kulia sana kwa ajili yako;

watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao

na kujivingirisha kwenye majivu.

31Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,

nao watavaa magunia.

Watakulilia kwa uchungu wa moyo

na kwa maombolezo makuu.

32Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,

watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:

“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,

katika moyo wa bahari?”

33Bidhaa zako zilipotoka baharini,

ulitosheleza mataifa mengi;

kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako

ulitajirisha wafalme wa dunia.

34Sasa umevunjavunjwa na bahari,

katika vilindi vya maji,

bidhaa zako na kundi lako lote

vimezama pamoja nawe.

35Wote wanaoishi katika nchi za pwani

wanakustaajabia;

wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,

nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.

36Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;

umefikia mwisho wa kutisha

nawe hutakuwepo tena.’ ”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help