Waebrania 1 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Mungu amesema kupitia Mwana

1Zamani, Mungu alisema na baba zetu kupitia kwa manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali,

2lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kupitia kwa Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu.

3Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Baada ya kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.

4Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

Mwana ni mkuu kuliko malaika

5Kwa maana ni kwa malaika yupi Mungu aliwahi kusema,

“Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuwa Baba yako”?

Au tena,

“Mimi nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa Mwanangu”?

6Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema,

“Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”

7Anaponena kuhusu malaika, anasema,

“Huwafanya malaika wake kuwa pepo,

watumishi wake kuwa miali ya moto.”

8Lakini kwa habari za Mwana asema,

“Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

kitadumu milele na milele,

nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

ya ufalme wako.

9Umependa haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako

kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

10Pia asema,

“Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,

nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

11Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu;

zote zitachakaa kama vazi.

12Utazikunjakunja kama joho,

nazo zitabadilishwa kama vazi.

Lakini wewe hubadiliki,

nayo miaka yako haikomi kamwe.”

13Je, ni kwa malaika yupi Mungu aliwahi kusema,

“Keti mkono wangu wa kuume,

hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako”?

14Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help