Mithali 19 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

1Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,

kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.

2Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa,

wala kufanya haraka na kuikosa njia.

3Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake

hata hivyo moyo wake humkasirikia Bwana.

4Mali huleta rafiki wengi,

bali rafiki wa mtu maskini humwacha.

5Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo hataachwa huru.

6Wengi hujipendekeza kwa mtawala

na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.

7Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote:

Je, rafiki zake watamkwepa kiasi gani!

Ingawa huwafuata kwa kuwasihi,

hawapatikani popote.

8Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe,

yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.

9Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo ataangamia.

10Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa,

itakuwa vibaya kiasi gani

kwa mtumwa kuwatawala wakuu.

11Hekima ya mtu humpa uvumilivu,

ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.

12Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba,

bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.

13Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye,

naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.

14Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,

bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.

15Uvivu huleta usingizi mzito,

naye mtu mzembe huona njaa.

16Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake,

bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.

17Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

naye atamtuza kwa aliyotenda.

18Mkanye mwanao, kwa maana kufanya hivyo kuna tumaini,

usiwe mshirika katika mauti yake.

19Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake,

kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.

20Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,

nawe mwishoni utakuwa na hekima.

21Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

22Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho,

afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

23Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima,

kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,

bila kuguswa na shida.

24Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!

25Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara,

mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.

26Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake

ni mwana aletaye aibu na fedheha.

27Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,

utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.

28Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu

na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.

29Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka

na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help