Zaburi 145 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 145Wimbo wa kusifu ukuu na wema wa MunguWimbo wa sifa. Wa Daudi.

1Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,

nitalisifu jina lako milele na milele.

2Kila siku nitakusifu

na kulitukuza jina lako milele na milele.

3 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

ukuu wake haupimiki.

4Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,

watasimulia matendo yako makuu.

5Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,

nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.

6Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha,

nami nitatangaza matendo yako makuu.

7Wataadhimisha wema wako mwingi,

na wataimba kwa shangwe kuhusu haki yako.

8 Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,

si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.

9 Bwana ni mwema kwa wote,

ana huruma kwa vyote alivyovifanya.

10Ee Bwana, vyote ulivyovifanya vitakusifu,

watakatifu wako watakutukuza.

11Watasimulia utukufu wa ufalme wako

na kusema kuhusu ukuu wako,

12ili watu wote wajue matendo yako makuu

na utukufu wa fahari ya ufalme wako.

13Ufalme wako ni ufalme wa milele,

mamlaka yako hudumu vizazi vyote.

Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

14 Bwana huwategemeza wote waangukao,

na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.

15Macho ya watu wote yanakutazama,

nawe huwapa chakula chao wakati wake.

16Waufumbua mkono wako,

watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.

17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

18 Bwana yu karibu na wote wamwitao,

karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.

19Huwatimizia wamchao matakwa yao,

husikia kilio chao na kuwaokoa.

20 Bwana huwalinda wote wanaompenda,

bali waovu wote atawaangamiza.

21Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana.

Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu

milele na milele.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help