1Msifuni Bwana.
Lisifuni jina la Bwana,
msifuni, enyi watumishi wa Bwana,
2ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Bwana,
katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
3Msifuni Bwana, kwa kuwa Bwana ni mwema,
liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.
4Kwa maana Bwana amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe,
Israeli kuwa hazina yake ya pekee.
5Ninajua ya kuwa Bwana ni mkuu,
kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote.
6 Bwana hufanya lolote apendalo,
mbinguni na duniani,
katika bahari na vilindi vyake vyote.
7Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia;
hupeleka miali ya radi pamoja na mvua
na huleta upepo kutoka ghala zake.
8Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,
mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama.
9Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri,
dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
10Aliyapiga mataifa mengi,
na akaua wafalme wenye nguvu:
11Mfalme Sihoni na Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani
na wafalme wote wa Kanaani:
12akatoa nchi yao kuwa urithi,
urithi kwa watu wake Israeli.
13Ee Bwana, jina lako ladumu milele,
kumbukumbu za fahari zako, Ee Bwana,
kwa vizazi vyote.
14Maana Bwana atawathibitisha watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake.
15Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
16Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
17zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.
18Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
19Ee nyumba ya Israeli, msifuni Bwana;
ee nyumba ya Haruni, msifuni Bwana;
20ee nyumba ya Lawi, msifuni Bwana;
ninyi mnaomcha, msifuni Bwana.
21Msifuni Bwana kutoka Sayuni,
msifuni yeye aishiye Yerusalemu.
Msifuni Bwana.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.