Matendo 3 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Petro amponya mlemavu kwa jina la Yesu

1Siku moja, Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali, yapata saa tisa alasiri.

2Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni.

3Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka.

4Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.”

5Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

6Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nitakachokupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!”

7Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu.

8Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu.

9Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu,

10wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu kwa yale yaliyomtukia.

Petro ashuhudia kuwa Yesu anaponya

11Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale Ukumbi wa Sulemani.

12Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea?

13Mungu wa Abrahamu na Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake.

14Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki, mkaomba mpewe yule muuaji.

15Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.

16Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni jina la Yesu na imani kutoka kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama nyote mnavyoona.

17“Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu.

18Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristo atateswa.

19Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kutoka kwake Bwana,

20naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu.

21Ilimpasa mbingu zimpokee hadi wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa manabii wake watakatifu.

22Kwa maana Musa alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia.

23Mtu ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’

24“Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi.

25Ninyi ndio wana wa manabii na wa agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’

26Mungu alipomfufua Yesu Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help