Kutoka Utangulizi - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025
UtanguliziNeno “Kutoka” linatokana na neno la Kiyunani “Exodos”, ambalo maana yake ni “Kutoka”, “Kuhama” au “Kuondoka”. Kitabu hiki kilipewa jina hili na watafsiri wa Agano la Kale kwa Kiyunani lijulikanalo kama “Septuagint” kwa sababu kinaelezea jinsi Waisraeli walivyoongozwa na Mungu kuondoka nchi ya Misri. Kitabu hiki kinaelezea mambo makubwa aliyoyafanya Mungu katika kuwaokoa Waisraeli kutoka maisha ya utumwa kule Misri. Huu ulikuwa ni muujiza mkubwa katika historia ya taifa la Israeli.Kutokana na maisha magumu waliyoishi Waisraeli utumwani huko Misri, Mungu alimchagua Musa kutekeleza mpango wake maalum wa ukombozi wa watu wake, yaani kuwaondoa utumwani Misri na kuwaongoza hadi nchi ya Kanaani, ambayo aliwaahidi baba zao.Mungu alionesha nguvu zake kwa Waisraeli na kwa Wamisri katika yale mapigo kumi. Pigo la mwisho lilisababisha Waisraeli waruhusiwe kuondoka Misri. Kabla ya Waisraeli kuondoka Misri waliadhimisha Sikukuu ya Pasaka. Tukio hili lilifanyika katika historia iliyofuata baadaye na kuandikwa katika vitabu vya Israeli.Waisraeli walianza safari ya kuondoka Misri wakiwa wanalindwa na kuongozwa na Mungu kupitia nguzo ya wingu wakati wa mchana, na nguzo ya moto wakati wa usiku. Walipofika Mlima Sinai, Mungu alifanya Agano lake na Waisraeli kwa kuwapa sheria za kuongoza maisha yao. Hapo Mlima Sinai, Musa alipewa ufunuo mkuu na wa pekee wa jinsi taifa la Israeli lilivyotakiwa kumtii na kumwabudu Mungu. Ufunuo huo ndio kiini na asili ya dini ya Kiyahudi.MwandishiMusa.KusudiKueleza jinsi Mungu alivyowakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwafanya kuwa taifa, na kisha kuanza safari ya kuenda Kanaani, nchi aliyowaahidi.MahaliWaisraeli wakiwa jangwani, katika Ghuba ya Sinai.TareheMnamo 1450–1410 K.K.Wahusika WakuuMusa, Haruni, Miriamu, Farao, Binti Farao, Yethro, Yoshua na Bezaleli.Wazo KuuKitabu cha Kutoka kinaelezea jinsi Waisraeli walivyoteswa, kunyanyaswa, na kugandamizwa wakiwa utumwani katika nchi ya Misri, kukombolewa kwao kwa uwezo wa Mungu, kufanyika kwa Agano kati yao na Mungu, kupewa Sheria, kujengwa kwa Hema, na mwanzo wa ukuhani wa Haruni.Mambo MuhimuKutolewa utumwani, na kuanzishwa kwa Pasaka; kuongozwa na Mungu kuvuka Bahari ya Shamu; kuingia kwenye Agano na Mungu; kuanzishwa kwa uhusiano baina ya Israeli na Mungu; kutolewa kwa Amri Kumi katika Mlima Sinai; na Israeli kutambuliwa kuwa taifa takatifu la Mungu lenye wajibu wa kumwabudu Mungu kwa moyo wote na kumtii.YaliyomoIsraeli wagandamizwa Misri, na Musa achaguliwa na Mungu (1:1–4:31)Ugumu wa Farao na matokeo yake (5:1–11:10)Kuanzishwa kwa Pasaka na pigo la mwisho (12:1‑30)Kutoka Misri hadi Mlima Sinai (12:31–18:27)Agano la Mungu na amri zake (19:1–24:18)Taratibu za ibada na dhabihu (25:1–40:38).