Zaburi 102 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 102Maombi ya mtu aliyechokaMaombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Bwana.

1Ee Bwana, usikie maombi yangu;

kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.

2Usinifiche uso wako

ninapokuwa katika shida.

Unitegee sikio lako;

ninapoita, unijibu kwa upesi.

3Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi;

mifupa yangu inaungua kama kaa la moto.

4Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani;

ninasahau kula chakula changu.

5Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu,

nimebakia ngozi na mifupa.

6Nimekuwa kama bundi wa jangwani,

kama bundi kwenye magofu.

7Nilalapo sipati usingizi;

nimekuwa kama ndege mpweke

kwenye paa la nyumba.

8Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki;

wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana.

9Ninakula majivu kama chakula changu,

nimechanganya kinywaji changu na machozi

10kwa sababu ya ghadhabu yako kuu,

kwa maana umeniinua na kunitupa kando.

11Siku zangu ni kama kivuli cha jioni,

ninanyauka kama jani.

12Lakini wewe, Ee Bwana, umeketi kwenye kiti chako cha enzi milele;

sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote.

13Utainuka na kuihurumia Sayuni,

kwa maana ni wakati wa kumwonesha wema;

wakati uliokubalika umewadia.

14Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako,

vumbi lake lenyewe hulionea huruma.

15Mataifa wataogopa jina la Bwana,

wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako.

16Kwa maana Bwana ataijenga tena Sayuni

na kutokea katika utukufu wake.

17Ataitikia maombi ya mtu mkiwa,

wala hatadharau hoja yao.

18Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho,

ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Bwana:

19“Bwana alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu,

alitazama dunia kutoka mbinguni,

20kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa,

na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.”

21Kwa hiyo jina la Bwana latangazwa huko Sayuni

na sifa zake katika Yerusalemu,

22wakati mataifa na falme zitakapokusanyika

ili kumwabudu Bwana.

23Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu,

akafupisha siku zangu.

24Ndipo niliposema:

“Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu;

miaka yako inaendelea vizazi vyote.

25Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia,

nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

26Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu,

zote zitachakaa kama vazi.

Utazibadilisha kama nguo

nazo zitaondoshwa.

27Lakini wewe, U yeye yule,

nayo miaka yako haikomi kamwe.

28Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako;

wazao wao wataimarishwa mbele zako.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help