Marko Utangulizi - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025
UtanguliziYohana Marko, mwandishi wa Injili hii, alitajwa na mababa wa Kanisa la kwanza, yaani Papiasi, Irenio na Klementi wa Iskanderia, kuwa mshirika wa karibu sana wa Mtume Petro. Yohana Marko alikuwa mtoto wa Mariamu, ambaye nyumba yake ilikuwa kituo kikuu cha Ukristo huko Yerusalemu. Hatimaye Marko aliishi Rumi ambako aliandika kumbukumbu za Mtume Petro.Marko alisafiri na mjomba wake, Barnaba, hadi Antiokia ya Siria walipofuatana na Paulo kwenye safari yake ya kwanza kueneza Injili. Hata hivyo, Marko aliwaacha Barnaba na Paulo huko Kipro na kurudi Yerusalemu. Baadaye Barnaba na Marko walielekea Kipro wakati Paulo alienda jimbo la Asia. Miaka kama kumi baadaye, Marko alikuwa pamoja na Paulo huko Rumi. Shabaha ya Marko ilikuwa kukusanya pamoja ujumbe wote wa Habari Njema ya Kristo kwa kifupi.MwandishiYohana Marko.KusudiKumtambulisha Yesu, kazi, na mafundisho yake.MahaliRumi.TareheMnamo 55–65 B.K.Wahusika WakuuYesu Kristo na wanafunzi wake, Pilato, na viongozi wa dini ya Kiyahudi.Wazo KuuMarko anamdhihirisha Bwana Yesu kuwa Mtumishi wa Mungu, na Mtu wa vitendo aliyekuja kuyatimiza mapenzi ya Mungu.Mambo MuhimuMarko anaanza kwa kueleza habari za huduma ya Bwana Yesu hadharani na mahubiri yake kuhusu Habari Njema za ufalme wa Mungu. Kisha anatoa wazi unabii kuhusu matazamio ya kifo cha Bwana Yesu. Hatimaye anaeleza jinsi Bwana Yesu alivyosulubiwa msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na alivyofufuliwa kutoka kwa wafu; pia maneno na maagizo yake ya mwisho kwa wanafunzi wake.YaliyomoHuduma ya Yohana Mbatizaji (1:1‑13)Huduma ya Yesu huko Galilaya (1:14–9:50)Safari ya kwenda Yerusalemu na matukio mjini (10:1–12:44)Unabii kuhusu mambo yajayo (13:1‑37)Kufa na kufufuka kwa Yesu (14:1–16:20).