Zaburi 30 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 30Maombi ya shukraniUtenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.

1Nitakutukuza wewe, Ee Bwana,

kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,

na hukuacha adui zangu

washangilie juu yangu.

2Ee Bwana Mungu wangu, nilikuita unisaidie

na wewe umeniponya.

3Ee Bwana, umenitoa Kuzimu,

umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.

4Mwimbieni Bwana, enyi watakatifu wake;

lisifuni jina lake takatifu.

5Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,

bali upendo wake hudumu siku zote.

Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,

lakini furaha huja asubuhi.

6Nilipofanikiwa nilisema,

“Sitatikiswa kamwe.”

7Ee Bwana, uliponijalia,

uliuimarisha mlima wangu,

lakini ulipouficha uso wako

nilifadhaika.

8Kwako wewe, Ee Bwana, niliita,

niliomba rehema kwa Bwana:

9“Kuna faida gani katika kuangamia kwangu,

katika kushuka kwangu shimoni?

Je, mavumbi yatakusifu?

Je, yatatangaza uaminifu wako?

10Ee Bwana, unisikie na kunihurumia;

Ee Bwana, uwe msaada wangu.”

11Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,

ulinivua gunia ukanivika shangwe,

12ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.

Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help