2 Wakorintho 11 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Paulo na mitume wa uongo

1Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo.

2Ninawaonea wivu, wivu wa kiungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.

3Lakini nina hofu kuwa, kama vile Hawa alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.

4Kwa sababu mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.

5Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu”.

6Inawezekana mimi si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.

7Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo?

8Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi.

9Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nilipopungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walitimiza mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia.

10Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili.

11Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda!

12Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

13Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.

14Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru.

15Kwa hiyo basi si ajabu kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

Paulo ajivunia mateso yake

16Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo.

17Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana angesema, bali kama mjinga.

18Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu.

19Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana!

20Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyangʼanya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya.

21Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!

Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo.

22Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu.

23Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi.

24Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja.

25Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa;

26nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.

27Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.

28Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote.

29Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?

30Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu.

31Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo.

32Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata.

33Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help