Zaburi 118 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 118Shukrani kwa ajili ya ushindi

1Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;

fadhili zake zadumu milele.

2Israeli na aseme sasa:

“Fadhili zake zadumu milele.”

3Nyumba ya Haruni na iseme sasa:

“Fadhili zake zadumu milele.”

4Wote wanaomcha Bwana na waseme sasa:

“Fadhili zake zadumu milele.”

5Wakati wa maumivu yangu makuu, nilimlilia Bwana,

naye akanijibu kwa kuniweka huru.

6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.

Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

7 Bwana yuko pamoja nami,

yeye ni msaidizi wangu.

Nitawatazama adui zangu

wakiwa wameshindwa.

8Ni bora kumkimbilia Bwana

kuliko kumtumainia mwanadamu.

9Ni bora kumkimbilia Bwana

kuliko kuwatumainia wakuu.

10Mataifa yote yalinizunguka,

lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

11Walinizunguka pande zote,

lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

12Walinizunguka kama kundi la nyuki,

lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo;

kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

13Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka,

lakini Bwana alinisaidia.

14 Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu,

yeye amefanyika wokovu wangu.

15Sauti za shangwe na ushindi

zinavuma kwenye hema za wenye haki:

“Mkono wa kuume wa Bwana

umetenda mambo makuu!

16Mkono wa kuume wa Bwana

umeinuliwa juu,

mkono wa kuume wa Bwana

umetenda mambo makuu!”

17Sitakufa, bali nitaishi,

nami nitayatangaza matendo ya Bwana.

18 Bwana ameniadhibu vikali,

lakini hakuniacha nife.

19Nifungulie malango ya haki,

nami nitaingia na kumshukuru Bwana.

20Hili ni lango la Bwana

ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.

21Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu,

umekuwa wokovu wangu.

22Jiwe walilolikataa waashi,

limekuwa jiwe kuu la pembeni.

23 Bwana ametenda hili,

nalo ni la kushangaza machoni petu.

24Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya,

tushangilie na kufurahi ndani yake.

25Ee Bwana, tuokoe,

Ee Bwana, utujalie mafanikio.

26Heri yule ajaye kwa jina la Bwana.

Kutoka nyumba ya Bwana tunakubariki.

27 Bwana ndiye Mungu,

naye ametuangazia nuru yake.

Mkiwa na matawi mkononi,

unganeni kwenye maandamano ya sikukuu

hadi kwenye pembe za madhabahu.

28Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,

wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.

29Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;

fadhili zake zadumu milele.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help