Mithali 24 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Msemo 20

1Usiwaonee wivu watu waovu,

usitamani ushirika nao;

2kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri,

nayo midomo yao husema kuhusu kuleta madhara.

Msemo 21

3Kwa hekima nyumba hujengwa,

nayo kupitia ufahamu huimarishwa;

4kwa maarifa vyumba vyake hujazwa

vitu vya thamani na vya kupendeza.

Msemo 22

5Mtu mwenye hekima ana uwezo mkubwa,

naye mtu mwenye maarifa huongeza nguvu,

6kwa kufanya vita unahitaji uongozi

na kwa ushindi washauri wengi.

Msemo 23

7Hekima i juu mno kwa mpumbavu,

katika kusanyiko langoni

hana lolote la kusema.

Msemo 24

8Yeye apangaye mabaya

atajulikana kama mtu wa hila.

9Mipango ya upumbavu ni dhambi,

watu huchukizwa na mwenye dhihaka.

Msemo 25

10Ukikata tamaa wakati wa taabu,

jinsi gani nguvu zako ni kidogo!

11Okoa wale wanaoongozwa kwenye kifo;

wazuie wote wanaojikokota

kuelekea machinjoni.

12Mkisema, “Lakini hatukujua lolote kuhusu hili,”

je, yule apimaye mioyo halitambui hili?

Je, yule awalindaye maisha yenu halijui hili?

Je, hatamlipa kila mtu kulingana na aliyotenda?

Msemo 26

13Ule asali mwanangu, kwa kuwa ni nzuri;

asali kutoka sega ni tamu kwa kuonja.

14Ujue pia kwamba hekima ni tamu kwa nafsi yako:

Ukiipata, kuna matumaini kwako ya siku zijazo,

nalo tumaini lako halitakatiliwa mbali.

Msemo 27

15Usivizie kama haramia afanyavyo ili kuyashambulia

makao ya mwenye haki,

wala usiyavamie makazi yake,

16kwa maana ingawa mtu mwenye haki huanguka mara saba,

huinuka tena;

lakini waovu huangushwa chini na maafa.

Msemo 28

17Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo;

wakati anapojikwaa,

usiruhusu moyo wako ushangilie.

18 Bwana asije akaona na kuchukia

akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.

Msemo 29

19Usikasirike kwa sababu ya wapotovu,

wala usiwaonee wivu waovu,

20kwa maana mpotovu hana tumaini la siku zijazo,

nayo taa ya waovu itazimwa.

Msemo 30

21Mwanangu, mche Bwana na mfalme,

wala usijiunge na waasi,

22kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao,

naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta?

Misemo zaidi ya wenye hekima

23Hii pia ni misemo ya wenye hekima:

Kuonesha upendeleo katika hukumu si vyema:

24Yeyote amwambiaye mwenye hatia,

“Wewe huna hatia,”

makabila ya watu watamlaani,

na mataifa watamkana.

25Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia,

nazo baraka tele zitawajilia juu yao.

26Jawabu la uaminifu

ni kama busu la mdomoni.

27Maliza kazi zako za nje,

nawe uweke mashamba yako tayari,

baada ya hayo, jenga nyumba yako.

28Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu,

au kutumia midomo yako kudanganya.

29Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda mimi;

nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea.”

30Nilipita karibu na shamba la mvivu,

karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,

31miiba ilikuwa imeota kila mahali,

ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na

ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.

32Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona,

nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:

33Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

34na umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,

na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help