Isaya 17 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Neno dhidi ya Dameski

1Neno la unabii kuhusu Dameski:

“Tazama, Dameski haitakuwa tena mji

bali itakuwa lundo la magofu.

2Miji ya Aroeri itaachwa

na itaachiwa mifugo ambayo italala huko,

bila yeyote wa kuyaogopesha.

3Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu,

nao uweza wa ufalme kutoka Dameski;

mabaki ya Aramu yatakuwa

kama utukufu wa Waisraeli,”

asema Bwana wa majeshi.

4“Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia,

unono wa mwili wake utadhoofika.

5Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka

na kuvuna nafaka kwa mikono yake,

kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke

katika Bonde la Warefai.

6Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki,

kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa,

kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni,

nne au tano katika matawi yanayozaa sana,”

asema Bwana, Mungu wa Israeli.

7Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao,

na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli.

8Hawataziangalia tena madhabahu,

kazi za mikono yao,

nao hawataheshimu nguzo za Ashera,

na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.

9Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.

10Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu,

hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu.

Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana

na kuotesha mizabibu ya kigeni,

11hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote

na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue,

hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu

katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka.

12Ole! Ghadhabu ya mataifa mengi:

wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka!

Ole! Makelele ya mataifa wanaovuma:

wanavuma kama ngurumo za maji mengi!

13Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo za maji yanayofanya mawimbi,

wakati anayakemea yanakimbia mbali,

yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima,

kama jani likivingirishwa na dhoruba.

14Wakati wa jioni, hofu ya ghafula!

Kabla ya asubuhi, wametoweka!

Hili ndilo fungu la wale wanaotupora,

fungu la wale wanaotunyangʼanya mali yetu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help