Mika 3 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Viongozi na manabii wakemewa

1Kisha nikasema,

“Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo,

enyi watawala wa nyumba ya Israeli.

Je, hampaswi kujua hukumu,

2ninyi mnaochukia mema

na kupenda maovu;

ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi

na kuondoa nyama kwenye mifupa yao;

3ninyi mnaokula nyama ya watu wangu,

mnaowachuna ngozi

na kuvunja mifupa yao vipande vipande;

mnaowakatakata kama nyama

ya kuwekwa kwenye sufuria

na kama nyama

ya kuwekwa kwenye chungu?”

4Kisha watamlilia Bwana,

lakini hatawajibu.

Wakati huo atawaficha uso wake

kwa sababu ya uovu waliotenda.

5Hili ndilo asemalo Bwana:

“Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu,

mtu akiwalisha,

wanatangaza ‘amani’;

kama hakufanya hivyo,

wanaandaa kupigana vita dhidi yake.

6Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono,

na giza, msiweze kubashiri.

Jua litawachwea manabii hao,

nao mchana utakuwa giza kwao.

7Waonaji wataaibika

na waaguzi watafedheheka.

Wote watafunika nyuso zao

kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”

8Lakini mimi nimejazwa nguvu,

nimejazwa Roho wa Bwana,

haki na uweza,

kumtangazia Yakobo kosa lake,

na Israeli dhambi yake.

9Sikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo,

enyi watawala wa nyumba ya Israeli,

mnaodharau haki

na kupotosha kila lililo sawa;

10mnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu

na Yerusalemu kwa uovu.

11Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa,

na makuhani wake wanafundisha kwa malipo,

nao manabii wake wanatabiri kwa fedha.

Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema,

“Je, Bwana si yumo miongoni mwetu?

Hakuna maafa yatakayotupata.”

12Kwa ajili yenu,

Sayuni italimwa kama shamba,

Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,

na kilima cha Hekalu

kitakuwa kichuguu

kilichofunikwa na vichaka.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help