Zaburi 140 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 140Kuomba ulinzi wa MunguKwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1Ee Bwana, niokoe, kutoka kwa watu waovu;

nilinde na watu wenye jeuri,

2ambao hupanga mipango mibaya mioyoni mwao,

na kuchochea vita siku zote.

3Wao hufanya ndimi zao kali kama za nyoka,

sumu ya nyoka iko midomoni mwao.

4Ee Bwana, niepushe na mikono ya waovu;

nilinde na watu wenye jeuri

wanaopanga kunikwaza miguu yangu.

5Wenye kiburi wameficha mtego wa kuninasa,

wametandaza kamba za wavu wao,

wametega mitego kwenye njia yangu.

6Ee Bwana, ninakuambia, “Wewe ni Mungu wangu.”

Ee Bwana, usikie kilio changu na kunihurumia.

7Ee Bwana Mwenyezi, Mwokozi wangu mwenye nguvu,

unikingaye kichwa changu siku ya vita:

8Ee Bwana, usiwape waovu matakwa yao,

usiache mipango yao ikafanikiwa,

wasije wakajisifu.

9Vichwa vya wanaonizunguka vifunikwe na shida

zilizosababishwa na midomo yao.

10Makaa ya mawe ya moto na yawaangukie!

Na watupwe motoni,

katika mashimo ya matope,

wasiinuke tena kamwe.

11Wasingiziaji wasifanikiwe katika nchi;

maafa na yawawinde watu wenye jeuri.

12Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki,

na kuitegemeza njia ya mhitaji.

13Hakika wenye haki watalisifu jina lako,

na waadilifu wataishi mbele zako.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help