Nahumu Utangulizi - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025
UtanguliziJina “Nahumu” maana yake ni “Faraja”. Nahumu alikuwa raia wa Elkoshi na alihudumu wakati mmoja na Sefania, Yeremia na Habakuki. Katika ujumbe wake alizungumzia kuanguka kwa Thebesi mwaka wa 663 K.K. na kuanguka kwa Ninawi mnamo mwaka wa 612 K.K. Ninawi, mji mkuu wa Ashuru, ulikuwa ni alama ya ukatili, mateso, hali ya kujilimbikizia mali, na utawala wa nguvu. Hii ndiyo sababu mji huu uliangushwa mwaka 621 K.K. Miaka michache kabla ya kuangushwa kwa mji wa Ninawi, Nabii Nahumu alitabiri kuhusu tukio hilo.Kitabu hiki kimehifadhi ujumbe mfupi wa Nahumu juu ya Ninawi. Katika unabii huu Nahumu anaelezea na kuonesha kuzingirwa na kuanguka kwa Ninawi kuwa ndio mwisho wa ufalme huu wa Ashuru. Kwa mantiki hiyo, Nahumu anawashauri watu wake kuzitii sikukuu zao za kidini, kwa kuwa Waashuru wasingeushambulia mji wa Yerusalemu tena. Ingawa ujumbe unaonesha ghadhabu ya Mungu dhidi ya Ninawi, ni muhimu sana ujumbe huu ukachukuliwa sambamba na ujumbe wa Nabii Yona kwamba Mungu aliupenda mji wa Ninawi.MwandishiNahumu.KusudiKutangaza hukumu ya Mungu dhidi ya Waashuru na kutoa ujumbe wa faraja kwa watu wa Yuda.MahaliNinawi.TareheMnamo 663–612 K.K.Wahusika WakuuWatu wa Ninawi na Waisraeli.Wazo KuuKuangamizwa kwa Ninawi na faraja kwa Waisraeli.Mambo MuhimuNahumu anaeleza kukaribia kwa hukumu ya Ninawi na jinsi itakavyokuwa kwa lugha ya wazi. Anaorodhesha kwa kifupi dhambi za Ninawi na kutamka kwamba Mungu ni mwenye haki katika hukumu zake. Anamalizia kwa kuiona hukumu iliyokamilika. Hiki ndicho kitabu cha Agano la Kale kinachotoa unabii wake waziwazi juu ya ukatili wa Waashuru.YaliyomoHasira ya Mungu dhidi ya Ninawi (1:1‑15)Kuanguka kwa Ninawi (2:1‑13)Ole wa Ninawi (3:1‑19).