Hesabu 20 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Maji kutoka mwamba(Kut 17:1‑7)

1Katika mwezi wa kwanza, jumuiya yote ya Waisraeli walifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.

2Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Musa na Haruni.

3Watu wakagombana na Musa, na kusema, “Laiti tungekufa ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana!

4Kwa nini mmewaleta jumuiya ya Bwana kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu?

5Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri hadi mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”

6Musa na Haruni wakaondoka pale kwenye kusanyiko hadi kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Bwana ukawatokea.

7Bwana akamwambia Musa,

8“Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Haruni mkawakusanye watu wote. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

9Kwa hiyo Musa akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza.

10Musa na Haruni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Musa akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?”

11Ndipo Musa akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

12Lakini Bwana akamwambia Musa na Haruni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”

13Haya yalikuwa maji ya Meriba, ambapo Waisraeli waligombana na Bwana, naye akajionesha kuwa mtakatifu kati yao.

Edomu wakatalia Israeli kupita

14Musa akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema:

“Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata.

15Baba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu,

16lakini tulipomlilia Bwana, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri.

“Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.

17Tafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lolote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kwenye kisima chochote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto hadi tuwe tumeshapita nchi yako.”

18Lakini mfalme wa Edomu akajibu:

“Hamtapita hapa. Mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”

19Waisraeli wakajibu:

“Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine chochote.”

20Watu wa Edomu wakajibu tena:

“Hamwezi kupita hapa.”

Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu.

21Kwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.

Kifo cha Haruni

22Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.

23Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu, Bwana akamwambia Musa na Haruni,

24“Haruni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba.

25Watwae Haruni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima Hori.

26Mvue Haruni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Haruni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”

27Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Waisraeli.

28Musa akamvua Haruni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Haruni akafia pale juu ya mlima. Kisha Musa na Eleazari wakateremka kutoka mlimani.

29Jumuiya yote walipofahamu kwamba Haruni amekufa, Waisraeli wote wakamwomboleza kwa siku thelathini.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help