1 Nyakati 23 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Jamaa za Walawi na utendaji wao

1Daudi alipokuwa mzee aliyeshiba siku, akamfanya Sulemani mwanawe kuwa mfalme juu ya Israeli.

2Pia akawakusanya viongozi wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi.

3Walawi waliokuwa na umri wa miaka thelathini au zaidi walihesabiwa, nayo hesabu ya wanaume ilikuwa elfu thelathini na nane.

4Daudi akasema, “Miongoni mwa hawa, elfu ishirini na nne watasimamia kazi ya Hekalu la Bwana na elfu sita watakuwa maafisa na waamuzi,

5na elfu nne watakuwa mabawabu, na wengine elfu nne watamsifu Bwana kwa ala za uimbaji nilizotoa kwa ajili ya kusudi hilo.”

6Daudi akawagawa Walawi katika makundi kufuatana na wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari.

Wagershoni

7Wana wa Wagershoni walikuwa wawili:

Ladani na Shimei.

8Wana wa Ladani walikuwa watatu:

Yehieli wa kwanza, Zethamu na Yoeli.

9Wana wa Shimei walikuwa watatu:

Shelomothi, Hazieli na Harani.

Hawa watatu walikuwa viongozi wa jamaa za Ladani.

10Nao wana wa Shimei walikuwa:

Yahathi, Zina, Yeushi na Beria.

Hawa walikuwa wana wa Shimei: wanne kwa jumla.

11Yahathi alikuwa wa kwanza na Ziza wa pili, lakini Yeushi na Beria hawakuwa na wana wengi; kwa hiyo walihesabiwa kama jamaa moja, wakapewa wajibu kwa pamoja.

Wakohathi

12Wana wa Kohathi walikuwa:

Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli: wanne kwa jumla.

13Wana wa Amramu walikuwa:

Haruni na Musa.

Haruni waliwekwa wakfu, yeye na wazao wake milele, wawe wakiweka wakfu vitu ambavyo ni vitakatifu mno, kutoa dhabihu mbele za Bwana, kuhudumu mbele zake na kubariki katika Jina la Bwana milele.

14Wana wa Musa mtu wa Mungu walihesabiwa kama sehemu ya kabila la Lawi.

15Wana wa Musa walikuwa:

Gershomu na Eliezeri.

16Wazao wa Gershomu:

Shebueli alikuwa wa kwanza.

17Wazao wa Eliezeri:

Rehabia alikuwa wa kwanza.

Eliezeri alikuwa na mwana mmoja tu, lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi sana.

18Wana wa Ishari:

Shelomithi alikuwa wa kwanza.

19Wana wa Hebroni walikuwa:

Yeria alikuwa wa kwanza, wa pili Amaria,

wa tatu Yahazieli, na wa nne Yekameamu.

20Wana wa Uzieli walikuwa:

Mika wa kwanza na Ishia wa pili.

Wamerari

21Wana wa Merari walikuwa:

Mahli na Mushi.

Wana wa Mahli walikuwa:

Eleazari na Kishi.

22Eleazari akafa bila ya kuwa na wana: alikuwa na binti tu. Binamu zao, wana wa Kishi, wakawaoa.

23Wana wa Mushi:

Mahli, Ederi na Yeremothi; wote walikuwa watatu.

24Hawa walikuwa wazao wa Lawi kwa jamaa zao. Wakuu wa jamaa kama walivyoandikwa kwa majina yao na kuhesabiwa kila mmoja, yaani wenye uwezo wa kufanya kazi kuanzia miaka ishirini au zaidi, waliohudumu katika Hekalu la Bwana.

25Kwa maana Daudi alikuwa amesema, “Kwa vile Bwana, Mungu wa Israeli, amewapa watu wake amani, na amekuja kuishi Yerusalemu milele,

26Walawi hawahitaji tena kubeba Maskani wala chombo chochote cha utumishi wake.”

27Kulingana na maagizo ya mwisho ya Daudi, Walawi walihesabiwa kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi.

28Wajibu wa Walawi ulikuwa kuwasaidia wazao wa Haruni kuhudumu katika Hekalu la Bwana: Kuwa wasimamizi wa nyua, vyumba vya pembeni, kutakasa vyombo vitakatifu na utendaji mwingine wowote katika nyumba ya Mungu.

29Walikuwa wasimamizi wa mikate iliyowekwa mezani, unga kwa ajili ya sadaka za nafaka, mikate myembamba isiyotiwa chachu, uokaji na uchanganyaji, pamoja na vipimo vyote vya wingi na ukubwa.

30Pia ulikuwa wajibu wao kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Bwana. Iliwapasa pia kufanya hivyo jioni

31na wakati wowote sadaka za kuteketezwa zilipotolewa kwa Bwana siku za Sabato na kwenye sikukuu za Mwezi Mwandamo na katika sikukuu nyingine zilizoamriwa. Iliwapasa kuhudumu mbele za Bwana mara kwa mara kwa idadi maalum na kwa namna waliyokuwa wamepewa maelekezo.

32Hivyo Walawi wakafanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, katika Mahali Patakatifu chini ya uongozi wa ndugu zao wazao wa Haruni, kwa ajili ya utumishi katika Hekalu la Bwana.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help