Zaburi 103 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 103Upendo wa MunguZaburi ya Daudi.

1Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Vyote vilivyo ndani yangu

vilihimidi jina lake takatifu.

2Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,

wala usisahau wema wake wote:

3akusamehe dhambi zako zote,

akuponya magonjwa yako yote,

4aukomboa uhai wako na kaburi,

akuvika taji la upendo na huruma,

5atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,

ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.

6 Bwana hutenda haki,

naye huwapa hukumu ya haki

wote wanaodhulumiwa.

7Alimjulisha Musa njia zake,

na watu wa Israeli matendo yake.

8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;

si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.

9Yeye hatalaumu siku zote,

wala haweki hasira yake milele,

10yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu

wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.

11Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia,

ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;

12kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,

ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.

13Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,

ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;

14kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,

anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.

15Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,

anachanua kama ua la kondeni;

16upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,

mahali pake hapalikumbuki tena.

17Lakini kutoka milele hata milele

upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao,

nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:

18kwa wale walishikao agano lake

na kukumbuka kuyatii mausia yake.

19 Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,

na ufalme wake unatawala vitu vyote.

20Mhimidini Bwana, enyi malaika wake,

ninyi mlio mashujaa, mnaozitii amri zake,

ninyi mnaotii neno lake.

21Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,

ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.

22Mhimidini Bwana, enyi kazi zake zote

kila mahali katika milki yake.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help