Zaburi 22 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 22Kilio cha uchungu na wimbo wa sifaKwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri”. Zaburi ya Daudi.

1Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?

Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?

2Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu,

hata usiku, sinyamazi.

3Hata hivyo umesimikwa kwenye kiti cha enzi,

Wewe Uliye Mtakatifu;

wewe ni sifa ya Israeli.

4Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao,

walikutumaini nawe ukawaokoa.

5Walikulilia wewe na ukawaokoa,

walikutegemea wewe nao hawakuaibika.

6Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu,

wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau.

7Wote wanaoniona wananidhihaki;

wananivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao:

8Wanasema, “Amtegemea Bwana,

basi Bwana na amwokoe.

Amkomboe basi, kwa maana

anapendezwa naye.”

9Hata hivyo ulinitoa tumboni,

ukanifanya nikutegemee,

hata nilipokuwa ninanyonya

matiti ya mama yangu.

10Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa,

toka tumboni mwa mama yangu

umekuwa Mungu wangu.

11Usiwe mbali nami,

kwa maana shida iko karibu

na hakuna wa kunisaidia.

12Mafahali wengi wamenizunguka,

mafahali wa Bashani wenye nguvu

wamenizingira.

13Simba wanaonguruma na kurarua mawindo

wanapanua vinywa vyao dhidi yangu.

14Nimemiminwa kama maji,

mifupa yangu yote imeteguka viungoni.

Moyo wangu umegeuka kuwa nta,

umeyeyuka ndani yangu.

15Nguvu zangu zimekauka kama kigae,

ulimi wangu umegandamana

na kaakaa la kinywa changu,

kwa sababu umenilaza

katika mavumbi ya kifo.

16Mbwa wamenizunguka,

kundi la watu waovu limenizingira;

wamenidunga mikono na miguu.

17Naweza kuhesabu mifupa yangu yote,

watu wananikodolea macho na kunisimanga.

18Wanagawana nguo zangu,

na vazi langu wanalipigia kura.

19Lakini wewe, Ee Bwana,

usiwe mbali.

Ee Nguvu yangu,

uje haraka unisaidie.

20Okoa maisha yangu na upanga,

uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa.

21Niokoe kutoka kinywani mwa simba,

niokoe kutoka pembe za nyati.

22Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu,

katika kusanyiko nitakusifu wewe.

23Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni!

Ninyi nyote wazao wa Yakobo, mheshimuni yeye!

Mcheni yeye, ninyi wazao wa Israeli!

24Kwa maana hakupuuza wala kudharau

mateso ya aliyeteswa;

hakumficha uso wake

bali alisikiliza kilio chake.

25Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa,

nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wanaokucha wewe.

26Maskini watakula na kushiba,

wale wanaomtafuta Bwana watamsifu:

mioyo yenu na iishi milele!

27Miisho yote ya dunia itakumbuka

na kumgeukia Bwana,

nazo jamaa zote za mataifa

zitasujudu mbele zake,

28kwa maana ufalme ni wa Bwana

naye huyatawala mataifa.

29Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu.

Wote wanaoshuka mavumbini

watapiga magoti mbele yake,

wote ambao hawawezi

kudumisha uhai wao.

30Wazao wa baadaye watamtumikia yeye;

vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana.

31Watatangaza haki yake kwa watu

ambao hawajazaliwa bado,

kwa maana yeye ametenda hili.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help