Zaburi 88 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 88Kilio kwa ajili ya kuomba msaadaWimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.

1Ee Bwana, Mungu uniokoaye,

nimelia mbele zako usiku na mchana.

2Maombi yangu yafike mbele zako,

utegee kilio changu sikio lako.

3Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,

na maisha yangu yanakaribia kaburi.

4Nimehesabiwa miongoni mwa wale wanaoshuka shimoni;

niko kama mtu asiye na nguvu.

5Nimetengwa pamoja na wafu,

kama waliochinjwa walalao kaburini,

ambao huwakumbuki tena,

ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.

6Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,

katika vina vya giza nene.

7Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,

umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.

8Umenitenga na rafiki zangu wa karibu

na kunifanya chukizo kwao.

Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;

9nuru ya macho yangu

imefifia kwa ajili ya huzuni.

Ee Bwana, ninakuita kila siku,

ninakunyooshea wewe mikono yangu.

10Je, wewe huwaonesha wafu maajabu yako?

Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?

11Je, upendo wako hutangazwa kaburini,

uaminifu wako katika Uharibifu?

12Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,

au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?

13Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana, unisaidie;

asubuhi maombi yangu huja mbele zako.

14Ee Bwana, kwa nini unanikataa

na kunificha uso wako?

15Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;

nimepatwa na mapigo yako, nami nimekata tamaa.

16Ghadhabu yako imepita juu yangu;

mapigo yako yameniangamiza.

17Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;

zimenimeza kabisa.

18Umeniondolea rafiki na wapendwa wangu;

giza limekuwa rafiki yangu wa karibu kuliko wote.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help