1Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwa Bwana. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya.
3Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Bwana na kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli.
4Akajenga miji katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na ngome na minara mwituni.
5Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta mia moja za fedha, kori elfu kumi za ngano, na kori elfu kumi za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.
6Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele za Bwana Mungu wake.
7Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
8Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita.
9Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.