Nehemia 1 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Maombi ya Nehemia

1Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia:

Katika mwezi wa Kislevu katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani,

2Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.

3Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”

4Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.

5Kisha nikasema:

“Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wanaompenda na kutii amri zake,

6tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako.

7Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Musa mtumishi wako.

8“Kumbuka agizo ulilompa Musa mtumishi wako, ukisema, ‘Mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa,

9lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali nilipopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’

10“Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu.

11Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.”

Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help