Amosi 8 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Maono ya nne: Kikapu cha matunda yaliyoiva

1Hili ndilo alilonionesha Bwana Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva.

2Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?”

Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.”

Ndipo Bwana akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”

3 Bwana Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”

4Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,

na kuwaonea maskini wa nchi,

5mkisema,

“Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita

ili tupate kuuza nafaka,

na Sabato itakwisha lini

ili tuweze kuuza ngano?”

Mkipunguza vipimo,

na kuongeza bei,

na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,

6mkiwanunua maskini kwa fedha,

na wahitaji kwa jozi ya viatu,

na mkiuza hata takataka za ngano

pamoja na ngano.

7 Bwana ameapa kwake mwenyewe, aliye Fahari ya Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya.

8“Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili,

nao wote wanaoishi ndani yake hawataomboleza?

Nchi yote itainuka kama Mto Naili;

itapanda na kushuka kama mto wa Misri.

9“Katika siku ile,” asema Bwana Mwenyezi,

“Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia

iwe giza wakati wa mchana mwangavu.

10Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo,

na kuimba kwenu kote kuwe kilio.

Nitawafanya ninyi nyote mvae magunia

na kunyoa nywele zenu.

Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee,

na mwisho wake kama siku ya uchungu.

11“Siku zinakuja,” asema Bwana Mwenyezi,

“wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote:

si njaa ya chakula wala kiu ya maji,

lakini njaa ya kusikia maneno ya Bwana.

12Wanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari

na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki,

wakitafuta neno la Bwana,

lakini hawatalipata.

13“Katika siku ile

“wasichana wazuri na wavulana wenye nguvu

watazimia kwa sababu ya kiu.

14Wale waapao kwa aibu ya Samaria,

au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’

au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’:

wataanguka, wala hawatasimama tena.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help