2 Wathesalonike 1 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Salamu

1Paulo, Silvano na Timotheo.

Kwa kanisa la Wathesalonike mlio katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

2Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi.

Shukrani na maombi

3Ndugu, inatupasa kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, na inastahili hivyo kwa sababu imani yenu inazidi kukua sana, nao upendo wa kila mmoja wenu kwa mwenzake unazidi kuongezeka.

4Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivunia saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

5Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili yake.

6Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,

7na kuwapa ninyi mnaoteseka amani pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atadhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu.

8Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu.

9Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake,

10siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

11Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu wetu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu.

12Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help