1Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi,
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lolote limpendezalo.
4Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
10Ee nyumba ya Haruni, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
11Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
12 Bwana anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Haruni,
13atawabariki wale wanaomcha Bwana,
wadogo kwa wakubwa.
14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15Mbarikiwe na Bwana
Muumba wa mbingu na dunia.
16Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17Sio wafu wanaomsifu Bwana,
wale wanaoshuka mahali pa kimya,
18bali ni sisi tunaomtukuza Bwana,
sasa na hata milele.
Msifuni Bwana.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.