Zaburi 116 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 116Shukrani kwa kuokolewa kutoka mauti

1Nampenda Bwana kwa maana amesikia sauti yangu;

amesikia kilio changu ili anihurumie.

2Kwa sababu amenitegea sikio lake,

nitamwita siku zote za maisha yangu.

3Kamba za mauti zilinizunguka,

vitisho vya Kuzimu vilinipata,

nikalemewa na taabu na huzuni.

4Ndipo nikaliitia jina la Bwana:

“Ee Bwana, niokoe!”

5 Bwana ni mwenye neema na haki,

Mungu wetu ni mwingi wa huruma.

6 Bwana huwalinda wanyenyekevu,

nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.

7Ee nafsi yangu, tulia tena,

kwa kuwa Bwana amekuwa mwema kwako.

8Kwa kuwa wewe, Ee Bwana,

umeniokoa nafsi yangu na mauti,

macho yangu kutokana na machozi,

miguu yangu kutokana na kujikwaa,

9ili niweze kutembea mbele za Bwana,

katika nchi ya walio hai.

10Nilimwamini Bwana, niliposema,

“Mimi nimeteseka sana.”

11Katika taabu yangu nilisema,

“Wanadamu wote ni waongo.”

12Nimrudishie Bwana nini

kwa wema wake wote alionitendea?

13Nitakiinua kikombe cha wokovu

na kulitangaza jina la Bwana.

14Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana

mbele za watu wake wote.

15Kifo cha watakatifu kina thamani

machoni pa Bwana.

16Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,

mimi ni mtumishi wako,

mwana wa mjakazi wako;

umeniweka huru

toka katika minyororo yangu.

17Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru

na kuliita jina la Bwana.

18Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana

mbele za watu wake wote,

19katika nyua za nyumba ya Bwana,

katikati yako, ee Yerusalemu.

Msifuni Bwana.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help