Zaburi 34 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 34Sifa na wema wa MunguZaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.

1Nitamtukuza Bwana nyakati zote,

sifa zake zitakuwa mdomoni mwangu siku zote.

2Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,

walioonewa watasikia na wafurahi.

3Mtukuzeni Bwana pamoja nami,

naam, na tulitukuze jina lake pamoja.

4Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,

akaniokoa kwenye hofu zangu zote.

5Wale wamtazamao hutiwa nuru,

nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

6Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,

akamwokoa katika taabu zake zote.

7Malaika wa Bwana hufanya kituo

akiwazunguka wale wamchao,

naye huwaokoa.

8Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema;

heri mtu yule anayemkimbilia.

9Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,

kwa maana wale wamchao

hawapungukiwi na chochote.

10Wana simba wenye nguvu

hutindikiwa na kuona njaa,

bali wale wanaomtafuta Bwana

hawatakosa kitu chochote kilicho chema.

11Njooni, watoto wangu, mnisikilize,

nitawafundisha kumcha Bwana.

12Yeyote kati yenu anayependa uzima

na kutamani kuziona siku nyingi njema,

13basi auzuie ulimi wake na mabaya,

na midomo yake kutokana na kusema uongo.

14Aache uovu, atende mema,

aitafute amani na kuifuatilia.

15Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.

16Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu,

ili kufuta kumbukumbu lao duniani.

17Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

huwaokoa katika taabu zao zote.

18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

na huwaokoa waliopondeka roho.

19Mwenye haki ana mateso mengi,

lakini Bwana humwokoa nayo yote,

20huhifadhi mifupa yake yote,

hata mmoja hautavunjika.

21Ubaya utamuua mtu mwovu,

nao adui za mwenye haki watahukumiwa.

22 Bwana huwakomboa watumishi wake,

yeyote anayemkimbilia yeye

hatahukumiwa kamwe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help