1Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,
nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2Nitafurahi na kushangilia ndani yako.
Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
3Adui zangu wamerudi nyuma,
wamejikwaa na kuangamia mbele zako.
4Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu;
umeketi kwenye kiti chako cha enzi,
ukihukumu kwa haki.
5Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu;
umeyafuta majina yao milele na milele.
6Uharibifu usiokoma umempata adui,
umeingʼoa miji yao;
hata kumbukumbu lao limetoweka.
7 Bwana anatawala milele,
ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki,
atatawala mataifa kwa haki.
9 Bwana ni kimbilio la wanaodhulumiwa,
ni ngome imara wakati wa shida.
10Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,
kwa maana wewe Bwana,
hujawaacha kamwe wanaokutafuta.
11Mwimbieni Bwana sifa, amefanywa mtawala Sayuni,
tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.
12Kwa maana yeye anayelipiza kisasi cha damu hukumbuka,
hapuuzi kilio cha wanaoonewa.
13Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi
adui zangu wanaonitesa!
Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,
14ili niweze kutangaza sifa zako
katika malango ya Binti Sayuni,
na huko niushangilie wokovu wako.
15Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba,
miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.
16 Bwana anajulikana kwa haki yake,
waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.
17Waovu wataishia Kuzimu,
naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
18Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,
wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.
19Ee Bwana, inuka, usimwache binadamu ashinde.
Mataifa na yahukumiwe mbele zako.
20Ee Bwana, wapige kwa hofu,
mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.