Marko 1 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Huduma ya Yohana Mbatizaji(Mk 1:1‑13)Yohana Mbatizaji atayarisha njia(Mt 3:1‑12; Lk 3:1‑8; Yn 1:19‑28)

1Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu,

2kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako”:

3“sauti ya mtu aliaye nyikani,

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyoosheni mapito yake.’”

4Yohana Mbatizaji alikuja akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

5Watu kutoka Yudea yote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

6Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Alikula nzige na asali ya mwitu.

7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake.

8Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu abatizwa(Mt 3:13‑17; Lk 3:21‑22)

9Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani.

10Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua.

11Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”

Yesu ajaribiwa nyikani(Mt 4:1‑11; Lk 4:1‑13)

12Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu hadi nyikani,

13naye Yesu akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama pori, nao malaika wakamhudumia.

Huduma ya Yesu huko Galilaya(Mk 1:14–9:50)Yesu aanza kuhubiri(Mt 4:12‑17; Lk 4:14‑15)

14Baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu alienda Galilaya, akaanza kuhubiri Habari Njema ya Mungu,

15akisema, “Wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Wanafunzi wa kwanza wa Yesu(Mt 4:18‑22; Lk 5:1‑11; Yn 1:35‑51)

16Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi.

17Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”

18Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.

19Alipoenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

20Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Yesu atoa pepo mchafu(Lk 4:31‑37)

21Wakaenda hadi Kapernaumu. Mara ilipofika siku ya Sabato, Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha.

22Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama walimu wa sheria.

23Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapaza sauti akisema,

24“Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

25Lakini Yesu akamkemea, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!”

26Yule pepo mchafu akamgaragaza huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

27Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

28Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Yesu amponya mama mkwe wa Simoni na pia watu wengi(Mt 8:14‑17; Lk 4:38‑41)

29Mara walipotoka katika sinagogi, walienda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani mwa Simoni na Andrea.

30Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake.

31Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

32Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu.

33Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo.

34Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.

Yesu aenda Galilaya(Lk 4:42‑44)

35Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba.

36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta,

37nao walipomwona, wakapaza sauti, wakasema, “Kila mtu anakutafuta!”

38Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine, kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia. Maana nilikuja kwa kusudi hili.”

39Kwa hiyo akazunguka Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Yesu amtakasa mtu mwenye ukoma(Mt 8:1‑4; Lk 5:12‑16)

40Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akapiga magoti, akimwomba, “Ukitaka, unaweza kunitakasa.”

41Yesu, akiwa amejawa na huruma, akaunyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!”

42Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.

43Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake mara moja;

44akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”

45Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi bali alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help