Hosea 5 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Hukumu dhidi ya Israeli

1“Sikieni hili, enyi makuhani!

Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli!

Sikieni, ee nyumba ya mfalme!

Hukumu hii ni dhidi yenu:

Mmekuwa mtego huko Mispa,

wavu uliotandwa juu ya Tabori.

2Waasi wamezidisha sana mauaji.

Mimi nitawatiisha wote.

3Ninajua yote kuhusu Efraimu,

Israeli hukufichika kwangu.

Efraimu, sasa umegeukia ukahaba,

Israeli amenajisika.

4“Matendo yao hayawaachii

kurudi kwa Mungu wao.

Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao,

hawamkubali Bwana.

5Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao;

Waisraeli, hata Efraimu,

wanajikwaa katika dhambi zao;

pia Yuda atajikwaa pamoja nao.

6Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ngʼombe

kumtafuta Bwana,

hawatampata;

yeye amejiondoa kutoka kwao.

7Wao si waaminifu kwa Bwana;

wamezaa watoto haramu.

Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi

zitawaangamiza wao

pamoja na mashamba yao.

8“Pigeni tarumbeta huko Gibea,

na baragumu huko Rama.

Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni;

ongoza, ee Benyamini.

9Efraimu ataachwa ukiwa

katika siku ya kuadhibiwa.

Miongoni mwa makabila ya Israeli

ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.

10Viongozi wa Yuda ni kama wale

wanaosogeza mawe ya mpaka.

Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao

kama mafuriko ya maji.

11Efraimu amedhulumiwa,

amekanyagwa katika hukumu

kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.

12Mimi ni kama nondo kwa Efraimu,

na kama uozo kwa watu wa Yuda.

13“Efraimu alipoona ugonjwa wake,

naye Yuda vidonda vyake,

ndipo Efraimu aligeukia Ashuru,

na kuomba msaada kwa mfalme mkuu.

Lakini hawezi kukuponya,

hawezi kukuponya vidonda vyako.

14Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu,

kama simba mkubwa kwa Yuda.

Nitawararua vipande vipande na kuondoka;

nitawachukua mbali,

na hakuna wa kuwaokoa.

15Kisha nitarudi mahali pangu

hadi watakapokubali kosa lao.

Nao watautafuta uso wangu;

katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help