Wimbo 3 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

1Usiku kucha kwenye kitanda changu

nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;

nilimtafuta, lakini sikumpata.

2Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,

katika barabara zake na viwanja;

nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.

Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.

3Walinzi walinikuta

walipokuwa wakizunguka mji.

Nikawauliza, “Je, mmemwona

yule moyo wangu umpendaye?”

4Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita

nilimpata yule moyo wangu umpendaye.

Nilimshika na sikumwachia aende

hadi nilipomleta katika nyumba ya mama yangu,

katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.

5Binti za Yerusalemu, ninawaagiza

kwa paa na kwa ayala wa shambani:

Msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

6Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani

kama nguzo ya moshi,

anayenukia manemane na uvumba

iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote

vya mfanyabiashara?

7Tazama! Ni gari la Sulemani

likisindikizwa na mashujaa sitini,

walio wakuu sana wa Israeli,

8wote wamevaa panga,

wote wazoefu katika vita,

kila mmoja na upanga wake pajani,

wamejiandaa kwa ajili ya vitisho vya usiku.

9Mfalme Sulemani alijitengenezea gari;

alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.

10Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha,

kitako chake kwa dhahabu.

Kiti chake kilipambwa kwa zambarau,

gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo

na binti za Yerusalemu.

11Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,

mkamtazame Mfalme Sulemani akiwa amevaa taji,

taji ambalo mama yake alimvika

siku ya arusi yake,

siku ambayo moyo wake ulishangilia.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help