Ayubu 35 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Elihu alaumu mtu kujiona kuwa mwenye haki

1Ndipo Elihu akasema:

2“Je, unadhani hili ni haki?

Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’

3Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata,

na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’

4“Ningependa nikujibu wewe

na rafiki zako walio nawe.

5Tazama juu mbinguni ukaone;

yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.

6Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu?

Kama dhambi zako zikiwa nyingi,

hilo linamfanyia nini Mungu?

7Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini,

au yeye anapokea nini mkononi kwako?

8Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe,

nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.

9“Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso;

huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu.

10Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu,

yeye anifanyaye niimbe usiku,

11yeye atufundishaye sisi zaidi ya wanyama wa nchi,

na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’

12Yeye hajibu wakati watu waliapo

kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.

13Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili;

Mwenyezi hayazingatii.

14Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza

wewe usemapo humwoni,

tena kwamba kesi yako iko mbele zake

na wewe lazima umngojee,

15pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu

wala haangalii uovu hata kidogo?

16Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana;

anaongea maneno mengi bila maarifa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help