1 Samweli Utangulizi - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025
UtanguliziKatika andiko la Kiebrania, vitabu vya 1 Samweli na 2 Samweli vilikuwa kitabu kimoja. Kugawanyika na kuwa vitabu viwili kulifanyika katika tafsiri ya “Septuagint” (yaani Agano la Kale la Kiyunani), ambayo iliviita “Kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Ufalme.” Kitabu cha 1 Samweli kinaanza kuelezea kuzaliwa kwa Samweli na mafundisho yake hekaluni. Kinaelezea jinsi alivyoiongoza Israeli kama nabii, kuhani na mwamuzi.Waisraeli walipotamani kuwa na mfalme, Samweli, kwa uongozi wa Mungu, alimtia Sauli mafuta kuwa mfalme wa kwanza wa Waisraeli. Lakini Sauli aliacha kumtii Mungu, naye Mungu akamkataa asiendelee kuwa mfalme. Kisha Mungu akamwongoza Samweli kumtia Daudi mafuta kwa siri kuwa mfalme mahali pa Sauli. Sehemu ya kitabu hiki iliyobaki inaelezea mapambano kati ya Sauli na Daudi.MwandishiInawezekana ni Samweli hadi mahali kifo chake kimenakiliwa; pia maandishi ya manabii Nathani na Gadi yamejumuishwa.KusudiKitabu cha 1 Samweli kinaonesha historia ya Israeli chini ya uongozi wa waamuzi, kuonesha mabadiliko ya uongozi katika Israeli kutoka mfumo wa uongozi wa waamuzi kwenda kwa uongozi wa wafalme, na kuweka kumbukumbu za maisha ya watu ambao kupitia kwao Masiya angezaliwa.MahaliKatika nchi ya Israeli.TareheWakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani.Wahusika WakuuEli, Hana, Samweli, Sauli, Yonathani, na Daudi.Wazo KuuKuanzishwa kwa ufalme wa Waisraeli, na vile huo ufalme uliendelea chini ya Mfalme Sauli na Daudi.Mambo MuhimuKitabu cha 1 Samweli kinaonesha kumomonyoka kwa maadili kwa waamuzi wakati wa Samweli; mwanzo wa kushindwa kwa ufalme wakati wa Sauli; Daudi kutiwa mafuta na kujaribiwa kwa uzoefu wake; na pia, mwisho wa Sauli.YaliyomoEli, kuhani na mwamuzi, na Samweli (1:1–7:17)Samweli na Sauli, viongozi wa Israeli (8:1–15:35)Mfalme Sauli, na Daudi (16:1–31:13).