Zaburi 27 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 27Sala ya kusifuZaburi ya Daudi.

1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

nimwogope nani?

Bwana ni ngome ya uzima wangu,

nimhofu nani?

2Waovu watakaposogea dhidi yangu

ili wale nyama yangu,

adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

watajikwaa na kuanguka.

3Hata jeshi linizingire pande zote,

moyo wangu hautaogopa;

hata vita vitokee dhidi yangu,

hata hapo nitakuwa na ujasiri.

4Jambo moja ninamwomba Bwana,

hili ndilo ninalolitafuta:

niweze kukaa nyumbani mwa Bwana

siku zote za maisha yangu,

niutazame uzuri wa Bwana

na kumtafuta hekaluni mwake.

5Kwa kuwa siku ya shida,

atanihifadhi salama katika maskani yake,

atanificha uvulini mwa hema lake,

na kuniweka juu kwenye mwamba.

6Kisha kichwa changu kitainuliwa

juu ya adui zangu wanaonizunguka.

Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;

nitamwimbia Bwana na kumsifu.

7Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana,

unihurumie na unijibu.

8Moyo wangu unasema kuhusu wewe,

“Utafute uso wake!”

Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”

9Usinifiche uso wako,

usimkatae mtumishi wako kwa hasira;

wewe umekuwa msaada wangu.

Usinikatae wala usiniache,

Ee Mungu Mwokozi wangu.

10Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha,

Bwana atanipokea.

11Nifundishe njia yako, Ee Bwana,

niongoze katika njia iliyo nyoofu,

kwa sababu ya watesi wangu.

12Usiniachilie kwa nia za adui zangu,

kwa maana mashahidi wa uongo

wameinuka dhidi yangu,

wakipumua ujeuri.

13Nami bado nina tumaini hili:

nitauona wema wa Bwana

katika nchi ya walio hai.

14Mngojee Bwana;

uwe hodari na mwenye moyo mkuu,

na umngojee Bwana.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help