Luka 2 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Kuzaliwa kwa Yesu(Mt 1:18‑25)

1Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi.

2(Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.)

3Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.

4Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi.

5Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito.

6Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia,

7naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.

Wachungaji na malaika

8Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku.

9Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu.

10Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote.

11Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo, Bwana.

12Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ngʼombe.”

13Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

14“Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,

na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

15Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”

16Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe.

17Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto.

18Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo.

19Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari.

20Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.

21Hata zilipotimia siku nane, uliokuwa wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilopewa na malaika kabla hajatungwa mimba.

Yesu apelekwa Hekaluni

22Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Sheria ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana

23(kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”),

24na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”.

25Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.

26Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana.

27Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria,

28ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:

29“Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,

sasa mruhusu mtumishi wako

aende kwa amani.

30Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,

31ulioweka tayari machoni pa watu wote,

32nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa

na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”

33Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto.

34Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake,

35ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”

36Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa.

37Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba.

38Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

39Yusufu na Mariamu walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya.

40Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akijawa na hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Kijana Yesu Hekaluni

41Kila mwaka Yusufu na Mariamu mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

42Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na mbili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.

43Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yusufu na Mariamu mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua.

44Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na rafiki zao.

45Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta.

46Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.

47Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa.

48Yusufu na Mariamu mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”

49Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”

50Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.

51Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.

52Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help