Zaburi 48 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Zaburi 48Sayuni, mji wa MunguWimbo. Zaburi ya wana wa Kora.

1 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

katika mji wa Mungu wetu,

mlima wake mtakatifu.

2Ni mzuri katika kuinuka juu kwake,

furaha ya dunia yote.

Kama vilele vya juu vya Safoni ni Mlima Sayuni,

mji wa Mfalme Mkuu.

3Mungu yuko katika ngome zake;

amejionesha mwenyewe kuwa ngome yake.

4Wafalme walipounganisha nguvu,

waliposonga mbele pamoja,

5walimwona, wakashangaa,

wakakimbia kwa hofu.

6Kutetemeka kuliwashika huko,

maumivu kama ya mwanamke

mwenye uchungu wa kuzaa.

7Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi

zilizovunjwa na upepo wa mashariki.

8Kama tulivyokuwa tumesikia,

ndivyo tulivyoona

katika mji wa Bwana wa majeshi,

katika mji wa Mungu wetu:

Mungu ataufanya uwe salama milele.

9Ee Mungu, hekaluni mwako

tunatafakari upendo wako usiokoma.

10Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,

sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,

mkono wako wa kuume umejazwa na haki.

11Mlima Sayuni unashangilia,

vijiji vya Yuda vinafurahi

kwa sababu ya hukumu zako.

12Tembeeni katika Sayuni,

uzungukeni mji,

hesabuni minara yake;

13yatafakarini vyema maboma yake,

angalieni ngome zake,

ili mpate kusimulia habari zake

kwa kizazi kijacho.

14Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;

atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help