Hesabu 12 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

Miriamu na Haruni wampinga Musa

1Miriamu na Haruni walianza kuzungumza dhidi ya Musa kwa sababu ya mke wake Mkushi, kwa kuwa alikuwa ameoa Mkushi.

2Waliuliza, “Je, Bwana amesema kupitia Musa peke yake? Je, hajasema kutupitia sisi pia?” Naye Bwana akasikia hili.

3(Basi Musa alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)

4Ghafula Bwana akawaambia Musa, Haruni na Miriamu, “Njooni katika Hema la Kukutania, ninyi nyote watatu.” Kwa hiyo wote watatu wakaenda.

5Kisha Bwana akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye ingilio la Hema, akawaita Haruni na Miriamu. Waliposogea mbele,

6Bwana akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu:

“Akiwepo nabii wa Bwana miongoni mwenu,

nitajifunua kwake kwa maono,

nitanena naye katika ndoto.

7Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Musa;

yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.

8Kwake nitanena naye uso kwa uso,

waziwazi wala si kwa mafumbo;

yeye ataona umbo la Bwana.

Kwa nini basi ninyi hamkuogopa

kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Musa?”

9Hasira ya Bwana ikawaka dhidi yao, akawaacha.

10Hilo wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, Miriamu akawa tayari ana ukoma, mweupe kama theluji. Haruni akamgeukia, akaona ana ukoma.

11Kisha Haruni akamwambia Musa, “Tafadhali, bwana wangu, usituhesabie dhambi hii ambayo tumeifanya kwa upumbavu.

12Usimwache awe kama mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa mfu, ambaye nusu ya mwili wake imeharibika hapo atokapo katika tumbo la mama yake.”

13Hivyo Musa akamlilia Bwana akisema, “Ee Mungu, nakuomba umponye!”

14 Bwana akamjibu Musa, “Je, kama baba yake angemtemea usoni, asingeona aibu kwa siku saba? Mfungie nje ya kambi kwa siku saba; baada ya hapo anaweza kurudishwa kambini.”

15Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba, nao watu hawakuendelea na safari hadi aliporudishwa kambini.

16Baada ya hayo, watu waliondoka Haserothi, wakapiga kambi katika Jangwa la Parani.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help