Wimbo 8 - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025

1Laiti ungekuwa kwangu kama ndugu wa kiume,

ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu!

Kisha, kama ningekukuta huko nje,

ningekubusu,

wala hakuna mtu yeyote angenidharau.

2Ningekuongoza na kukuleta

katika nyumba ya mama yangu,

yeye ambaye amenifundisha.

Ningekupa divai iliyokolezwa unywe,

asali ya maua ya mikomamanga yangu.

3Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,

na mkono wake wa kuume unanikumbatia.

4Binti za Yerusalemu, ninawaagiza:

msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

Rafiki

5Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani

akimwegemea mpenzi wake?

Mpendwa

Nilikuamsha chini ya mtofaa,

huko mama yako alipotunga mimba yako,

huko yeye alipata uchungu akakuzaa.

6Nitie kama muhuri moyoni mwako,

kama muhuri kwenye mkono wako;

kwa maana upendo una nguvu kama mauti,

wivu wake ni mkatili kama Kuzimu.

Unachoma kama mwali wa moto,

kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa.

7Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,

mito haiwezi kuugharikisha.

Kama mtu angetoa mali yote ya nyumbani mwake

kwa ajili ya upendo,

angedharauliwa kabisa.

Rafiki

8Tunaye dada mdogo,

matiti yake hayajakua bado.

Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu

wakati atakapokuja kuposwa?

9Kama yeye ni ukuta,

tutajenga minara ya fedha juu yake.

Na kama yeye ni mlango,

tutamzungushia mbao za mwerezi.

Mpendwa

10Mimi ni ukuta,

nayo matiti yangu ni kama minara.

Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake

kama yule anayeleta utoshelevu.

11Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni;

alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji.

Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake

shekeli elfu moja za fedha.

12Lakini shamba langu la mizabibu

ambalo ni langu mwenyewe

ni langu kutoa;

hizo shekeli elfu moja ni kwa ajili yako, ee Sulemani,

na shekeli mia mbili ni kwa ajili

ya wale wanaotunza matunda yake.

Mpenzi

13Wewe ukaaye bustanini

pamoja na rafiki mliohudhuria,

hebu nisikie sauti yako!

Mpendwa

14Njoo, mpenzi wangu,

uwe kama paa

au kama ayala mchanga

juu ya milima iliyojaa manukato.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help