Isaya Utangulizi - Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu) 2025
UtanguliziJina Isaya maana yake ni “Bwana anaokoa”. Kufuatana na mapokeo, Isaya alitoa unabii wakati mmoja na Amosi, Hosea na Mika. Isaya alianza huduma yake mnamo 740 K.K. Isaya alikuwa ameoa, na akapata watoto wawili, Shear-Yashubu na Maher-Shalal-Hash-Bazi. Yamkini, Isaya alitumia wakati wake mwingi huko Yerusalemu wakati wa Mfalme Hezekia. Kufuatana na historia ya Kiyahudi, Isaya aliuawa kwa kupasuliwa vipande viwili chini ya utawala wa Manase, yule mwana mwovu wa Mfalme Hezekia, aliyetawala mnamo 696–642 K.K.MwandishiIsaya mwana wa Amozi.KusudiIsaya anatoa wito kwa taifa la Yuda kumrudia Mungu, na pia anawatangazia wokovu wa Mungu kupitia kwa Masiya.MahaliYerusalemu.TareheMnamo 700–680 K.K.Wahusika WakuuIsaya, wanawe wawili Shear-Yashubu na Maher-Shalal-Hash-Bazi, Mfalme Hezekia, na watu wa Yerusalemu na Yuda.Wazo KuuKuufanya ujumbe wa Mungu uwe wazi kwa Israeli, ili kuwaonya kuhusu hukumu ikiwa wataendelea kudumu katika dhambi. Pia kudhihirisha jinsi Mungu atakavyoshughulika nao katika kuwarejesha chini ya Masiya wao milele.Mambo MuhimuMungu atamtuma Masiya ili kuokoa watu wake; atakuja kama Mwokozi na Bwana pekee, lakini atatenda kama mtumishi. Atakufa ili kuziondoa dhambi. Mungu anaahidi kutuma faraja, ukombozi na urejesho katika ufalme wake ujao. Masiya atawatawala wafuasi wake wakati huo. Tumaini ni hakika kwa sababu Kristo yuaja.YaliyomoHukumu na matumaini ya kurejeshwa (1:1–6:13)Ishara mbalimbali kwa Israeli, ahadi ya kurejeshwa (7:1–12:6)Unabii dhidi ya mataifa (13:1–23:18)Hukumu ya Israeli na ukombozi (24:1–27:13)Maonyo, na Sayuni kutengenezwa (28:1–35:10)Mfalme Hezekia, Ashuru na Babeli (36:1–39:8)Ahadi za ukombozi wa Mungu (40:1–56:8)Ukombozi, faraja na utukufu wa wakati ujao (56:9–66:24).