Yoshua Mwana wa Sira 47 - Swahili Revised Union Version DC

Nathani

1 2 Sam 7:2-3; 12:1 Baada yake akasimama Nathani ili atoe unabii zamani za Daudi.

Daudi

2 1 Sam 17:34—18:7; 2 Sam 5:7; 8:1; 12:13 Kama mafuta yalivyotengwa na kafara ya amani, vivyo hivyo Daudi alitengwa na wana wa Israeli.

3Naye alicheza pamoja na simba kana kwamba ni wana-mbuzi, pia pamoja na dubu kana kwamba ni wana-kondoo wa kundi.

4Je! Hakumwua jitu katika ujana wake,

Akawaondolea watu lawama;

Alipouinua mkono wake na jiwe la teo,

Akayashusha majivuno ya Goliathi?

5Kwa maana alimwita Aliye Juu;

Na yeye akaitia nguvu yamini yake;

Ili amwue shujaa hodari wa vita;

Ili aiinue pembe ya watu wake.

6Kwa hiyo binti za watu wakamtukuza wakiimbiana, na kumheshimu alivyoua makumi elfu yake; naye alipokwisha kuivaa taji la utukufu,

7alipigana na adui na kuwashinda pande zote; akajenga maboma yake kati ya Wafilisti, akaivunja pembe yao vipande vipande, hata siku hii ya leo.

8Katika kila kazi yake Daudi alimshukuru Mungu Aliye Juu kwa maneno matukufu; na kwa moyo wake wote akampenda Mola wake, akamhimidi kila siku daima.

9Pia akaweka waimbaji mbele ya madhabahu, ili watoe sauti tamu katika kuimba kwao.

10Akauongeza uzuri wa sikukuu, akaziratibisha nyakati katika ukamilifu; pindi walipolihimidi jina takatifu la BWANA, hata patakatifu pakavuma sauti tokea asubuhi na mapema.

11Naye BWANA akamwondolea dhambi zake, akiinua pembe yake hata milele; akampa agano la ufalme, na kiti kitakatifu cha enzi katika Israeli.

Sulemani

12Na kwa ajili yake akainuliwa mwanawe, mtu wa ufahamu aliyekaa salama.

131 Fal 4:21-32 Sulemani alimiliki katika siku za kufanikiwa; naye Mungu akampa raha kumzunguka pande zote; ili alijengee jina lake nyumba, na kumwekea tayari patakatifu pa milele.

14Jinsi ulivyohekimishwa ujanani,

Na kujazwa ufahamu kama Nile!

15Nafsi yako uliifunikiza nchi,

Na kuikusanya mifano kama bahari.

16Jina lako likafikia visiwa vya mbali,

Nao wakaisikilizia habari yako;

17Kwa nyimbo, na mithali, na tafsiri,

Ukawastaajabisha watu wote.

18 1 Fal 10:21,27 Katika jina la BWANA Mungu,

Aitwaye Mungu wa Israeli,

Ulikusanya dhahabu kama chuma,

Na kuzidisha fedha kama mawe.

19 1 Fal 11:1 Ila kwa wanawake uliinamisha viuno,

Na kutiishwa mwili wako;

20Hivyo uliitupa heshima yako,

Na kukinajisi kitanda chako.

Uliwaletea wanao ghadhabu;

Kuna sikitiko kwa upuzi wako;

21 1 Fal 12:15-20 Hata ufalme ukagawanyika,

Wakatawala waasi katika Efraimu.

22 1 Sam 7:15 Bali BWANA hataiacha rehema yake,

Wala kulivunja neno lake;

Hatawafuta wazao wa mteule wake,

Wala kuharibu uzao wa mpenzi wake.

Basi, akamjalia Yakobo mabaki, na Daudi shina limtokalo.

Rehoboamu na Yeroboamu

23 1 Fal 11:43; 12:10-30; 2 Fal 17:6,18 Naye Sulemani akastarehe pamoja na baba zake. Huyo ndiye aliyemwacha nyuma yake, katika wazao wake, Rehoboamu, mpumbavu kabisa, asiyekuwa na ufahamu hata kidogo; ambaye aliwachukiza watu kwa shauri lake hata wakaasi.

Yeroboamu

24Yeroboamu mwana wa Nebati naye, aliyewakosesha Israeli, akawapatia Waefraimu kikwazo, hata wafukuzwe katika nchi yao. Tena dhambi zao zikaongezeka mno ajabu;

25mradi walijiuza kutenda kila namna ya uovu, hata kisasi kiwaangukie.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help