Mithali 10 - Swahili Revised Union Version DC

KITABU CHA PILIMithali za Sulemani

1Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;

Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.

2 Zab 49:6; Lk 12:19; Dan 4:27 Hazina za uovu hazifaidii kitu;

Bali haki huokoa na mauti.

3 Zab 10:14 BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa;

Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.

4 Mit 13:4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini;

Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.

5Akusanyaye wakati wa joto ni mwana mwenye hekima;

Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.

6 Est 7:8 Baraka humkalia mwenye haki kichwani;

Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.

7 Zab 9:5,6; Mhu 8:10 Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka;

Bali jina la mtu mwovu litaoza.

8Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo;

Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

9 Zab 23:4; Isa 33:15,16 Aendaye kwa unyofu huenda salama;

Bali apotoshaye njia zake atajulikana.

10Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko;

Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

11 Zab 37:30; 107:42 Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima;

Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,

12 Yak 5:20; 1 Pet 4:8; 1 Kor 13:4 Kuchukiana huleta fitina;

Bali kupendana husitiri makosa yote.

13 Lk 4:22 Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu;

Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.

14Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa;

Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.

15 Ayu 31:24; Mit 18:11; Lk 12:19; 1 Tim 6:17 Mali ya tajiri ndio ngome yake;

Ufukara wa maskini ndio umwangamizao.

16Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima;

Mazao ya wabaya huielekea dhambi.

17Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima;

Bali yeye aachaye maonyo hukosa.

18Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo,

Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.

19 Mhu 5:3; Zab 39:1; Mit 17:27,28; Yak 1:19 Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu;

Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.

20Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha safi;

Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.

21Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi;

Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.

22 Mwa 12:2; Kum 8:17,18; 1 Sam 2:7,8; 1 Tim 4:8 Baraka ya BWANA hutajirisha,

Wala hachanganyi huzuni nayo.

23Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo;

Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.

24 Ayu 15:21; Mt 5:6 Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;

Na wenye haki watapewa matakwa yao.

25 Zab 15:5; Mt 7:24; 1 Tim 6:19 Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena;

Bali mwenye haki ni msingi wa milele.

26Kama siki menoni, na kama moshi machoni,

Ndivyo alivyo mtu mvivu kwa hao waliomwajiri.

27 Mhu 7:17 Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu;

Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.

28 Zab 16:9; Rum 5:2; Ayu 8:13 Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha;

Bali matarajio yao wasio haki yatapotea.

29 Zek 10:12; Flp 4:13; Isa 40:31; Zab 1:6 Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu;

Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.

30Mwenye haki hataondolewa milele;

Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.

31Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima;

Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.

32Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa;

Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help