Zaburi 73 - Swahili Revised Union Version DC

KITABU CHA TATUOmbi la kuponywa kutoka kwa waonevuZaburi ya Asafu

1Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,

Kwa hao walio safi mioyo yao.

2Nami miguu yangu ilikuwa karibu kupotoka,

Hatua zangu zilikuwa karibu kuteleza.

3Maana niliwaonea wivu wenye kujivuna,

Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.

4Maana hawana maumivu katika kufa kwao,

Na miili yao ina nguvu.

5Hawana taabu kama watu wengine,

Wala hawapati mapigo kama wanadamu wenzao.

6 Mhu 8:11 Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao,

Udhalimu huwavika kama nguo.

7Macho yao hutokeza kwa kunenepa,

Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.

8 2 Pet 2:18; Yud 1:16 Hudhihaki, husimulia mabaya,

Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.

9 Ufu 13:6 Wameweka kinywa chao mbinguni,

Na ulimi wao hutangatanga duniani.

10Kwa hiyo watu wake hugeuka huko,

Na maji yaliyojaa humezwa nao.

11 Ayu 22:13; Zab 94:7 Nao husema, Mungu ajuaje?

Yako maarifa kwake aliye juu?

12Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki,

Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.

13 Ayu 21:15; Zab 24:4; Mal 3:14; Ebr 10:19-22 Hakika nimejisafisha moyo wangu bure,

Na kunawa mikono yangu nisitende dhambi.

14Maana mchana kutwa nimepigwa,

Na kuadhibiwa kila asubuhi.

15Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo;

Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.

16 Mhu 8:17 Nami nilifikiri jinsi ya kufahamu hayo;

Ikawa taabu machoni pangu;

17 Zab 77:13 Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu,

Nikautafakari mwisho wao.

18Hakika Wewe huwaweka penye utelezi,

Huwaangusha mpaka palipoharibika.

19Namna gani wameangamizwa punde!

Wakafutiliwa mbali kwa vitisho.

20Ee Bwana, wamekuwa kama ndoto wakati wa kuamka,

Uondokapo utaidharau sanamu yao.

21Moyo wangu ulipoona uchungu,

Viuno vyangu viliponichoma,

22Nilikuwa kama mjinga, sijui neno;

Nilikuwa kama mnyama tu mbele zako.

23Walakini mimi ni pamoja nawe daima,

Umenishika mkono wa kulia.

24 Isa 58:8; Yn 14:3; 2 Kor 5:1 Utaniongoza kwa shauri lako,

Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu.

25 Isa 26:8,9; Hab 3:17,18 Ni nani niliye naye mbinguni,

Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.

26 Zab 84:2 Mwili wangu na moyo wangu hupunguka,

Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu

Na sehemu yangu milele.

27Maana wajitengao nawe watapotea;

Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe.

28 Ebr 10:22 Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu;

Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU,

Niyahubiri matendo yako yote.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help