Wafilipi 2 - Swahili Revised Union Version

Kuiga unyenyekevu wa Kristo

1Basi ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako matulizo yoyote ya mapenzi, ukiwako ushirika wowote wa Roho, ikiwako huruma yoyote na rehema,

2ijalizeni furaha yangu, ili muwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkiwaza mamoja.

3Gal 5:26; Rum 12:10 Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

41 Kor 10:24,33 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

5Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6Yn 1:1,2; 17:5; Mwa 1:27; 3:5 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuko na namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7Isa 53:3; 2 Kor 8:9; Ebr 2:14,17 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8Ebr 12:2; 5:8; Yn 10:17 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

9Mdo 2:33; Efe 1:21; Ebr 1:3,4 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

10Isa 45:23; Yn 5:23; Ufu 5:13 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

11na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Kuangaza kama mianga ulimwenguni

12 1 Pet 1:17; Zab 2:11 Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

13Yn 15:5; 2 Kor 3:5; 1 The 2:13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.

14 1 Pet 4:9 Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,

15Kum 32:5; Mt 5:14; 10:16; Flp 1:10; Efe 5:8; Kum 32:5; Mdo 2:40 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,

161 The 2:19; Gal 2:2; Isa 49:4; 65:23 mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure.

17Rum 15:16; 2 Tim 4:6 Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote.

18Flp 3:1; 4:4 Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.

Timotheo na Epafrodito

19Lakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu.

201 Kor 16:10 Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli.

212 Tim 4:10,16; Gal 4:17 Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.

22Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake.

23Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata.

24Flp 1:25 Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibuni.

25 Flp 4:18 Lakini niliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mfanyakazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu.

26Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa mgonjwa.

27Kwa maana alikuwa mgonjwa sana, karibu kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni.

28Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu.

291 Kor 16:16; 1 Tim 5:17 Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa.

30Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akahatarisha roho yake ili kusudi aitimize huduma ambayo msingeweza kunitimizia.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help