1 Isa 47:7; Omb 1:9; Ezr 4:20 Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa,
Huo uliokuwa umejaa watu!
Jinsi alivyokuwa kama mjane,
Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa!
Binti mfalme kati ya majimbo,
Jinsi alivyoshikwa shokoa!
2 Yer 13:17; Omb 1:16; Ayu 7:3; Zab 6:6; Yer 4:30 Hulia sana wakati wa usiku,
Na machozi yake yapo mashavuni;
Miongoni mwa wote waliompenda
Hakuna hata mmoja amfarijiye;
Rafiki zake wote wamemtenda hila,
Wamekuwa adui zake.
3 Law 26:14,32,33; Kum 28:64 Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa,
Na kwa sababu ya utumwa mkuu;
Anakaa kati ya mataifa,
Haoni raha yoyote;
Wote waliomfuata wamempata
Katika dhiki yake.
4Njia za Sayuni zaomboleza,
Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu;
Malango yake yote yamekuwa ukiwa,
Makuhani wake hupiga kite;
Wanawali wake wanahuzunika;
Na yeye mwenyewe huona uchungu.
5 Yer 30:14; Omb 3:39 Watesi wake wamekuwa kichwa,
Adui zake hufanikiwa;
Kwa kuwa BWANA amemtesa
Kwa sababu ya wingi wa makosa yake;
Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka
Mbele yake huyo mtesi.
6Naye huyo binti Sayuni
Enzi yake yote imemwacha;
Wakuu wake wamekuwa kama ayala
Wasioona malisho;
Nao wamekwenda zao hawana nguvu
Mbele yake anayewafuatia.
7 Mik 4:11 Siku za mateso na misiba yake,
Yerusalemu huyakumbuka matamanio yake yote
Yaliyokuwa tangu siku za kale;
Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi,
Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia;
Hao watesi wake walimwona,
Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.
8 Yer 13:22 Yerusalemu amefanya dhambi sana;
Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu;
Wote waliomheshimu wanamdharau,
Kwa sababu wameuona uchi wake;
Naam, yeye anaugua,
Na kujigeuza aende nyuma.
9 Kum 32:29 Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake;
Hakukumbuka mwisho wake;
Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu;
Yeye hana mtu wa kumfariji;
Tazama, BWANA, mateso yangu;
Maana huyo adui amejitukuza.
10 Kum 23:3; Neh 13:1 Huyo mtesi amenyosha mkono wake
Juu ya matamanio yake yote;
Maana ameona ya kuwa mataifa wameingia
Ndani ya patakatifu pake;
Ambao kwa habari zao wewe uliamuru
Wasiingie katika kusanyiko lako.
11 Yer 38:9 Watu wake wote hupiga kite,
Wanatafuta chakula;
Wameyatoa matamanio yao wapate chakula
Cha kuihuisha nafsi;
Ee BWANA, tazama, uangalie;
Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.
12 Dan 9:12; Mt 24:21; Lk 21:22 Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia,
Angalieni, mtazame
Kama kuna majonzi yoyote mfano wa majonzi yangu,
Niliyotendwa mimi,
Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo
Siku ya hasira yake iwakayo.
13 Ayu 18:8; Zab 66:11; Eze 12:13; Hos 7:12 Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu,
Nao umeishinda;
Ametandika wavu aninase miguu,
Amenirudisha nyuma;
Amenifanya kuwa mtu wa pekee,
Na mgonjwa mchana kutwa.
14 Kum 28:48; Mit 5:22; Isa 14:25; Mt 11:29,30 Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake;
Hayo yameshikamana;
Yamepanda juu shingoni mwangu;
Amezikomesha nguvu zangu;
15 Isa 63:3; Ufu 14:19 Bwana amenitia mikononi mwao,
Ambao siwezi kupingamana nao.
Bwana amewafanya mashujaa wangu wote
Kuwa si kitu kati yangu;
Ameita mkutano mkuu kinyume changu
Ili kuwaponda vijana wangu;
Bwana amemkanyaga kama shinikizoni
Huyo bikira binti Yuda.
16Mimi ninayalilia mambo hayo;
Jicho langu, jicho langu linachuruzika machozi;
Kwa kuwa mfariji yuko mbali nami,
Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi;
Watoto wangu wameachwa peke yao,
Kwa sababu huyo adui ameshinda.
17Sayuni huinyosha mikono yake;
Hakuna hata mmoja wa kumfariji;
BWANA ametoa amri juu ya Yakobo,
Kwamba wamzungukao wawe watesi wake;
Yerusalemu amekuwa kati yao
Kama kitu kichafu.
18 Neh 9:33; Dan 9:7; 1 Sam 12:14 BWANA ndiye mwenye haki;
Maana nimeiasi amri yake;
Sikieni, nawasihi, enyi watu wote,
Mkayatazame majonzi yangu;
Wasichana wangu na wavulana wangu
Wamechukuliwa mateka.
19Niliwaita hao walionipenda
Lakini walinidanganya;
Makuhani wangu na wazee wangu
Walifariki mjini;
Hapo walipokuwa wakitafuta chakula
ili kuzihuisha nafsi zao.
20 Isa 16:11; Yer 4:19; Hos 11:8; Kum 32:25 Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki;
Mtima wangu umetaabika;
Moyo wangu umegeuka ndani yangu;
Maana nimeasi vibaya sana;
Huko nje upanga huua watu;
Nyumbani mna kama mauti.
21 Yer 46:1 Wamesikia kwamba napiga kite;
Hakuna hata mmoja wa kunifariji;
Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata;
Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo;
Utaileta siku ile uliyoitangaza,
Nao watakuwa kama mimi.
22Huo uovu wao wote
Na uje mbele zako wewe;
Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi
Kwa dhambi zangu zote;
Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana,
Na moyo wangu umezimia.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.